habari Mpya


Wakulima Ngara,Waishukuru Serikali kwa Kukomesha Walanguzi wa Kahawa.

Wakulima wa zao la Kahawa ,Kata ya Kirushya katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, wameishukuru Serikali  kuwaepusha na wahujumu wa kahawa,kwa madai kwamba msimu huu wanaweza kunufaika na zao hilo.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Mwivuza Bw. BaduluhTwaha, amesema wakulima mwaka huu watanufaika na zao hili, baada ya serikali kuwapiga faini walanguzi waliokiuka agizo la kutonunua kahawa ikiwa shambani.

Serikali ina nguvu na uwezo mkubwa bwana! kwani wale wote waliokuwa wamenunua kahawa ikiwa bado shambani kwa kutanguliza fedha, hivisasa wakipewa kahawa kama fidia wanakataa wanataka warejeshewe fedha yao.”Alisema Bw. Twaha.

Amefafanua kwamba walanguzi wa kahawa walikuwa wanawadhurumu wakulima, kwani mkulima akipewa labda shilingi 300,000/= mlanguzi anapata faida mara tatu ya malipo aliyomlipa mkulima.

Naye Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika  Wilaya ya Ngara , Bw.Constantine Mudende, amekiri kwamba wakulima mwaka huu watanufaika, kwani watalipwa kulingana na soko la wakati huo, na kwamba kila mmoja atatamani kulima zao hili kufuatia bei nzuri.

Amesema wakulima katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara wawe na subira, kwa madai kwamba msimu huu Ngara Famaers Cooperative wanatarajia kutumia zaidi ya shilingi bilioni 2 kununua kahawa ya wakulima wilayani humo.

Amesema wamefanya mazungumzo na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ili wapewe zaidi ya bilioni 2, kwa ajili ya kununulia kahawa na kwamba mazungumzo yanaendelea vizuri.

Afisa Kilimo huyo wa Wilaya ya Ngara amesema msimu ulitakiwa kuwa umeanza mwezi Mei 01, 2018; akaongeza kwamba wataanza kununua  kahawa hiyo muda wowote kuanzia sasa.

Post a Comment

0 Comments