habari Mpya


Shilingi Milioni 506 kutumika Kuboresha Mazingira ya Kufundishia na Kujifunzia wilayani Ngara mkoani Kagera.

Na Shaaban Ndyamukama, RK FM.

Halmashauri ya wilaya ya Ngara mkoani kagera inatarajia kutumia Sh506 milioni  kuboresha mazingira ya kufundishia  na kujifunzia   baada ya kuzipokea kutoka serikalini  kutokana na changamoto zinazojiktokeza kutokana na elimu bila malipo.

Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ngara ambaye pia ni Afisa elimu idara ya msingi  Gidion Mwesiga amesema fedha hizo zitatumika katika ujenzi wa vyumba vya madarasa matundu ya vyoo na kuboresha  nyumba za walimu.

Mwesiga amesema kati ya fedha hizo kiasi cha Sh142 milioni zitatumika  kujenga vyumba vya madarasa 30 na Sh153 milioni  zitajenga maabara katika shule tisa za sekondari wilayani humo na kiasi kingine  kitaboresha  sekta ya utawala.

Aidha Afisa elimu huyo amekiri kuwepo kwa Changamoto ya baadhi ya wanafunzi kutostahimili  stadi za kuhesabu kusoma na kuandika na kwamba utafiti uliofanywa na Twaweza  Uwezo  utafanyiwa kazi kuongeza ufaulu kitaaluma.

Alisema  utafiti huo umechelewa kutoa  matokeo kwani serikali  mpaka sasa ilishabaini  changamoto za KKK katika shule za msingi na kutoa mafunzo kwa walimu wa darasa la awali hadi la tatu mkoani Dodoma.

‘’Hivi sasa tunahitaji vitabu vya masomo ya darasa la nne kwa mtaala mpya ambapo vimeanza kusambazwa kwa mkoa wa pwani nasi tunatarajia kuvipokea makao makuu ya mkoa wetu wa Kagera hivi karibuni’’ Alisema Mwesiga.

Alidai kwamba utafiti huo utasaidia kutia hamasa kwa walimu kufanya kazi kwa kujituma wakitumia juhudi na maarifa hatimaye kuwafanya wanafunzi wajengewe msingi wa kufaulu kwa kiwango kinachokubalika.

Hata hivyo alishauri  wazazi kufuatilia watoyo wao kitaaluma kwa kushiriki vikao vya shule kamati na mikutano ya wazazi kwa kutoa mahitaji muhimu kama sare ya shule chakula na idara itahusika kuhamasisha walimu kutimiza wajibu wao kiutendaji kwa kutumia miongozo ya udhibiti ubora wa elimu. 

Hivi karibuni Idara ya elimu ya msingi wilayani Ngara ilitakiwa  kuboresha kiwango cha elimu  baada ya utafiti kubaini   wanafunzi  wa darasa la tatu ufaulu wao ni  wastani wa silimia 31 kwa  masomo ya Kiswahili, Kiingereza na Hisabati.

Mkurugenzi  wa Shirika la Marafiki wa Afrika Tanzania  Padre Isaias Bambara alibainisha hayo    wakati wa uzinduzi wa ripoti ya tathimini ya utafiti wa  uwezo kielimu iliyofanyika mwaka 2015 wilayani Ngara kwa  wanafunzi wenye umri wa miaka 9-13 kwa masomo hayo.

Padre Bambara alisema utafiti huo ulihusisha wanafunzi 112,455 kwa nchi nzima kati ya hao wilaya ya Ngara ilikuwa na wanafunzi 21, 800 waliokuwa katika kaya 60 ambapo kila kituo cha utafiti kilishirikisha wanafunzi 30.

Alisema  wanafunzi wa darasa la tatu wanaoweza kufanya hesabu ya darasa la pili ni asilimia 43, wenye kuweza kusoma hadithi ya kiswahili kwa  darasa la pili ni asilimia 67 na walioko  darasa la saba wanaoweza kufanya hesabu za darasa la pili ni wastani wa asilimia 53.

Aidha alisema darasa la saba wanaoweza kusoma hadithi za kiingereza kwa darasa la pili ni asilimia 42 huku  wenye kuweza kusoma hadithi za kiingereza kwa darasa ambapo mahudhurio ya walimu kazini  wilayani humo wastani wa asilimia 84 huku wanafunzi wakihudhuria masomo kwa wastani wa asilimia 52.

 "Wajibu wetu ni kushirikiana kuongeza ufaulu na ubora wa elimu kitaifa, kimkoa na kiwilaya na kwa kutumia utafiti huu tunaweza kuboresha miundombinu katika mazingira ya kufundishia na kujifunzia" Amesema Bambara.

Aidha amesema shirika la marafiki wa Afrika Tanzania (MAT) katika utafiti huo limetumia  jumla ya Sh19.9 milioni zilitumika ambapo shirika la Twaweza uwezo limetoa kiasi cha Sh1.3 milioni kuandaa ripoti na kuizindua.

Post a Comment

0 Comments