habari Mpya


Serikali ya wilaya ya Ngara yatoa Ardhi Ekari 1000 kwa Mwekezaji wa Kikorea.


Mwekezaji huyo WON DAE KIM akisalimiana na Wananchi wa Kijiji cha Kazingati.

Serikali ya wilaya ya Ngara mkoani Kagera imetoa ardhi ekari 1000 kwa ajili ya mwekezaji kutoka nchi ya Korea ya Kusini atakayejishughulisha na kilimo cha kahawa kisha kuwekeza kiwanda cha mbolea katika kijiji cha Kazingati kata ya Keza wilayani Ngara.

Mwekezaji huyo WON DAE KIM ni Mkurugenzi mkuu wa Kampuni ya FRIUP iliyoko Korea Kusini inayojihusisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa lengo la kuinua uchumi na kuharakisha maendeleo nchini humo.

Akizungumza May 13, 2018 baada ya kutembelea ardhi aliyopewa akiambatana na Viongozi wa wa wilaya ya Ngara katika kijiji cha Kazingati WON DAE KIM amesema uwekezaji huo utaambatana na ujenzi miundombinu kama barabara ,madaraja, na kuboresha vyanzo.

Pia aliomba Serikali ya wilaya hiyo kumuongezea eneo la ekari 8000 kwa ajili ya upanuzi wa kilimo cha mpunga na viazi mviringo baada ya kuridhika na eneo hilo kuwa na rutuba.

"Ninashukuru kwa ardhi hii imejaa maji na inaonesha rutuba nitahitaji ushirikiano wa wananchi kwa miradi itakayoanzishwa mazao yake soko kubwa ni kuanzia nchi za afrika mashariki na dunia kwa ujumla. "Alisema Kim
Mwekezaji huyo WON DAE KIM akiwa Ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngara,Mkoani Kagera.

Naye mwakilishi wake katika wilaya ya Ngara Issa Samma alisema baada ya mradi kuanza kutapatikana nafasi za ajira za muda na kudumu 2000 na kuendelea na maeneo mengine zitatumika mashine zenye kuhitaji wafanyakazi wa kusafisha mashamba.

Samma alisema katika eneo la uwekezaji limepimwa pia kwa ajili ya ujenzi wa reli na kwamba wananchi wajiandae kwa ajira na kufanya hata shughuli ,biashara kutokana na wingi wa watu ambao watakajitokeza nje na ndani ya nchi.

Akisaini Kitabu cha Wageni Kijiji cha Kazingati.
Mkurugenzi katikati akizungumza.

Aidha Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara Aidan Bahama alisema wilaya hiyo iko mita 1200 hadi 1800 kutoka usawa wa bahari na upatikanaji wa mvua ni mara mbili kwa mwaka kuanzia mililmita 800 ukanda wa chini na milimita 1400 ukanda juu inayotosheleza kilimo cha Kahawa. 

Kijiji cha Kazingati kilichotoa eneo la uwekezaji kina ardhi ekari 22,456 sawa na hekta 8,982 ambapo zao hilo hustawi ukanda wa tarafa ya Rulenge lilipo hilo enao alilopewa. 

Bahama alisema wilaya nzima ardhi inayofaa kwa kilimo ni hekta 303,483 na kwamba eneo linalobaki hutumika kwa ufugaji na shughuli nyingine hivyo uwekezaji huo utaongeza fursa ya ukisanyaji mapato. 

Wilaya ya Ngara ina kilomita za mraba 3,744 sawa na hekta 374,400 yenye wastani wa joto 18℅ mpaka 30℅ ikiwa na vijiji 75 vilivyopo ndani ya kata 22 kati ya hizo 19 zinalima zao la Kahawa. 


Na Shaaban Ndyamukama Radio Kwizera- NGARA

Post a Comment

0 Comments