habari Mpya


NMB yatoa Msaada wa Shilingi Milioni 20 Kuboresha Huduma za Jamii Mkoani Kagera.

Na: Sylvester Raphael-Kagera.

Benki ya NMB Mkoani Kagera yatoa misaada ya Shilingi Milioni 20,000,000/=  ya Vifaa Tiba na Samani kwa ajili ya Shule za Msingi na Sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba na Manispaa ya Bukoba ili kuboresha huduma za Jamii katika Halmashauri hizo.
 
Misaada hiyo imetolewa mapema leo Mei 25, 2018 katika Zahanati ya Nyanga Manispaa ya Bukoba ambapo katika Zahanati hiyo Benki ya NMB Mkoa wa Kagera ilitoa Vitanda 6, Magodaro 6, Vitanda viwili vya kujifungulia Wajawazito na Boksi moja la vifaa vya vinavyotumika wakati wa kujifungua akinamama, vifaa tiba hivyo vikiwa na thamani ya shilingi milioni 5,000,000/=.
 
Aidha, Benki hiyo ilitoa Madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 10,000,000/= katika shule za Msingi Kyaitoke na Kitwe kila shule madawati 50. Pia Shule ya Sekondari Bukara ilipokea viti 60 na meza 60 vyenye thamani ya shilingi milioni 5,000,000/= kutoka katika Benki hiyo na kukamilisha jumla ya shilingi milioni 20,000,000/=.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum  Kijuu (kushoto) akipokea Msaada kutoka kwa Meneja wa Kanda ya Ziwa Bw. Abraham Augustine (kulia) uliotolewa na Benki ya NMB Mkoani Kagera katika Zahanati ya Nyanga Manispaa ya Bukoba leo May 25, 2018.
Picha ya Pamoja.
 
Akikabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meneja wa Kanda ya Ziwa Bw. Abraham Augustine alisema kuwa Benki ya NMB imeamua makusudi kujikita katika kuhudumia jamii hasa katika Sekta za Elimu na Afya ili kuigusa jamii ya Watanzania moja kwa moja.
 
Bw. Augustine aliongeza kuwa katika mwaka huu 2018 Benki hiyo imetenga shilingi Bilioni 1 kwaajili ya kuihudumia jamii na tayari misaada mbalimbali imeishatolewa katika Sekta za Elimu na Afya yenye thamani ya shilingi Milioni 100 na mkoa wa Kagera tayari umenufanika.
 
Bw. Augustine alimalizia kwa kusema kuwa Benk ya NMB inarudisha faida inayoipata kwa wananchi kutokana na biashara wanayoifanya ili kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na faida hiyo hasa kupitia huduma za kijamii katika Sekta za Elimu na Afya.
Mara baada ya kupokea misaada hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum  Kijuu aliishukura sana Benki ya NMB kwa kurudisha faida kwa wananchi kupitia kutoa misaada ya kuboresha huduma za jamii kama Afya na Elimu.
 
Mhe. Kijuu alitoa wito kwa Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Serikali na yasiyokuwa ya Seriakli hasa Taasisi za Kibenki  kuiga mfano mzuri wa Benki ya NMB kwa kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za kijamii kama shule na Sekta ya Afya ili wananchi wapate huduma bora.
 
Mkuu a Mkoa Kijuu alitolea mfano Sekta ya Elimu kuwa baada ya Serikali kutoa Sera ya Elimu bila malipo kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wazazi kuwaandikisha wanafunzi kwa wingi katika shule jambo ambalo linaifanya miundombinu iliyokuwepo hapo awali kuonekana kuwa ni michache kwahiyo Serikali kwa kishirikiana na wananchi na wadau wengine wote wanatakiwa kuiboresha miundombinu hiyo ili kukidhi uhuhitaji ili huduma bora itolewe.
Aidha, Mara baada ya kupokea msaada wa meza na viti meza kwaniaba ya Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Kashasha aliishukuru benki ya NMB na kusema kwamba msaada huo umewafikia kwa wakati muafaka ulipokuwa unahitajika.
 
Naye Mhe. Jimmy Kalugendo Naibu Meya wa Manispaa ya Bukoba alisema kuwa Vifaa Tiba vilivyotolewa na Benki ya NMB Katika zahanati ya Nyanga ni msaada mkubwa katika kituo hicho kwani vifa atiba hivyo vilikuwa vimekwamisha Zahanati kufunguliwa lakini sasa itafunguliwa na kuanza kutoa huduma bora kwa wananchi wa eneo hilo.
 
Mkoa wa Kagera unayo matawi 22 ya Benki ya NMB na tawi la mwisho kufunguliwa ni Tawi la Kabanga Wilayani Ngara na kuna uwezekano wa Tawi lingine kufunguliwa Kamachumu Wilayani Muleba ili kutoa huduma kwa wananchi wa Nshamba, Rubya na Kamachumu .

Post a Comment

0 Comments