habari Mpya


Mkuu wa Mkoa wa Kagera Avikagua Vyama Vikuu Vya Ushirika Kuona Utayari wa Kukusanya Kahawa ya Wakulima Msimu Unapofunguliwa Juni Mosi 2018.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Akikagua Mashine za Kukoboa Kahawa Katika Kiwanda cha BUKOP.

Na: Sylvester Raphael.

Mkoa wa Kagera ukiwa mzalishaji mkubwa wa zao Kahawa nchini kwa zaidi ya asilimia 50 sasa wafanya maandalizi ya kufungua msimu wa mwaka huu 2018 wa ununuzi wa Kahawa kwa wakulima kupitia Vyama Vikuu  vya Ushirika vya Kagera Cooperative Union 1990 Limited (KCU 1990 LTD) na Karagwe District Co operative Union  Limited (KDCU LTD).

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu katika kuhakikisha agizo la Serikali la Wakulima kuuza Kahawa yao kupita Vyama vya Ushirika linatekelezwa kikamilifu amevitembelea Vyama Vikuu vya Ushirika vya KDCU Ltd  na KCU 1990 LTD kuona maandalizi ya kupokea kahawa hasa maghara ya kuhifadhi kahawa hizo pamajoa na viwnda vya kukoboa kama vipo tayari kufanya kazi msimu unapofunguliwa  Juni 1, 2018.

 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Akikagua Kahawa Iliyokoborewa Katika Ghara la Kiwanda cha BUKOP.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Kijuu alitembelea na kukagua mashine za kukoboa kahawa katika kiwanda  cha BUKOP na maghara ya kuhifadhi kahawa kiwandani hapo na ghara la Kemondo la KCU 1990 Ltd. 

Katika Mashine ya kukoboa kahawa BUKOP Mkuu wa Mkoa alijonea ukarabati wa mashine zilizomo katika kiwanda hicho zikifanyiwa ukarabati ili kuanza msimu wa ukoboaji

 
 
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Akiwa Katika Chama Cha Msingi Iteera Wilayani Kyerwa Kukagua Ghara la Kupokea Kahawa.

Katika Wilaya ya Karagwe Mkuu wa Mkoa alitembelea maghara ya Chama Kikuu cha KDCU Ltd pamoja na mashine ya kukoboa kahawa iliyokuwa ikifanyiwa ukarabati ambapo alipewa taarifa ya kiwanda hicho kudaiwa fedha za Ankara ya umeme na TANESCO ambapo alisema kuwa tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama inalifanyia kazi suala hilo ili msimu ukifunguliwa mashine hiyo iweze kukoboa kahawa.

Katika Wilaya ya Kyewa Mkuu wa Mkoa  alitembelea na kukagua maghara ya vyama vya Msingi vya Iteera na Karongo na kuridhika na maandalizi ya maghara hayo kupokea kahawa kwa msimu huu wa mwaka 2018 unaotarajiwa kufunguliwa Juni 1, 2018.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalaama ya Karagwe Akikagua Ghara la Chama Kikuu cha KDCU LTD.

Akiongea na viongozi wa Vyama hivyo Vikuu vya Ushirika Mkoani Kagera  Mhe. Kijuu alisema kuwa ni lazima mkoa usimamie agizo la Serikali,  na lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha wakulima wa kahawa wananufaika na kilimo chao cha kahawa bila kunyonywa. 

Aidha, alisistiza kuwa wakulima watapewa malipo ya awali na baada ya kahawa kuuzwa watalipwa malipo ya pili kulingana na bei ya soko la dunia.

“Najua wakulima wengi  wana mashaka na mfumo mpya wa uuzaji wa kahawa kutokana na makovu waliyoyapataa huko miaka ya nyuma lakini Serikali sasa imeamua kuhakikisha wananufaika na kahawa yao kupitia Vyama vya Ushirika na ndiyo maana nimeamua kufuatilia kwa karibu. 

Hapa namsafishia njia Mhe. Waziri Mkuu ambaye anatarajia kuja Kagera kuhakikisha mkulima ananufaika na Kahawa yake.” Alisistaiza Mhe. Kijuu.

Kahawa ambayo Tayari Imekomaa na Inasubiria Kuvunwa.

Maagizo; 

Mara baada ya kukagua maghara na viwanda vya kukoboa kahawa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu aliwaagiza Viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika  vya KCU Ltd na KDU Ltd kwanza  kuhakikisha maghara yanasafishwa kwa kiwango cha kuridhisha ili kupokea kahawa ya wakulima. 

Pili, kuhakikisha mizani yote inafanyiwa uhakiki na Wakala wa Vipimo kabla ya kuanza kukusanya kahawa ili mkulima asipunjwe katika vipimo.

Tatu, kukamilisha ukarabati wa mashine za kukoboa kahawa kwa wakati ili mara kahawa ikianza kukusanywa isikwame kukoborewa na kusababisha kucheleweshwa kwenda katika soko la mnada wa dunia na kuchelewesha malipo ya pili ya mkulima.

Nne, Kamati za Ulinzi na Usalama  za Wilaya kuhakikisha hakuna kahawa inauzwa “Obutura” wala kutoroshwa kwenda nchi jirani kwa wafanyabiashara  wanaonunua kwa njia ya magendo bila kusajilijiwa kihalali kama Vyama vya Ushirika vinavyotambulika.

Chama Kikuu cha KCU 1990 Ltd kinatarajia kukusanya tani 5,000 za kahawa maganda katika msimu huu wa mwaka 2018. Aidha, KDU Ltd inatarajia kukusanya kahawa ya wakulima kiasi cha tani 40,000 na asilimia 90 ya kahawa hiyo itakuwa Robusta na Arabika asilimia 10, pia katika kahawa hiyo kutakuwa na kahawa ya masoko maalum (Organic Coffee) tani 4,000.

Post a Comment

0 Comments