habari


Mei Mosi Mkoani Kagera Yaadhimishwa kwa Mafanikio Makubwa licha ya Kuwepo Mvua.

Maandamano ya Wafanyakazi Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wakielekea uwanja wa Mayunga mjini humo leo Mei 01,2018 kwa ajili ya Sherehe za Mei Mosi ambapo kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

 Na Shaaban Ndyamukama Radio Kwizera Bukoba.

Jumla ya wafanyakazi 66 kutoka idara mbalimbali za serikali za mitaa katika halmashauri nane za mkoa wa Kagera, wamepatiwa zawadi na  vyeti baada ya kubainika kuwa wafanyakazi bora kwa kuonesha nidhamu na kutimiza majukumu yao kiutendaji.

Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za mitaa mkoani Kagera TALGU Bw.Sunday Nzaligo alisema kati ya wafanyakazi hao hawakujumuishwa walioko sekta ya elimu kwa sababu hao ni watumishi wanaosimamiwa na  serikali kuu. 

Bw.Nzaligo alisema pamoja na kupatikana  zawadi za wafanyakazi bora, bado watuumishi wa serikali za mitaa mkoani Kagera wanaidai serikali Sh 4 bilioni  ambazo ni maslahi ya kiutendaji ndani na nje ya muda wa kazi.

Alisema pia wafanyakazi wa mkoa wa kagera wakiwa sawa na mikoa mingine nchini  wanakabiliwa na changamoto ya kufanya kazi kwa muda mrefu bila kupata nyongeza ya posho muda wa ziada kutokana na zoezi la kupunguza watumishi waliokuwa na vyeti vya kughushi.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni kuunganisha mifuko ya jamii kulenga kuboresha mafao ya wafanyakazi na kupata haki zao kwa mujibu wa sheria baada ya kutimiza wajibu kwa mwajiri” Alisema Nzoliga.

Maandamano ya Wafanyakazi Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wakielekea uwanja wa Mayunga mjini humo leo Mei 01,2018 kwa ajili ya Sherehe za Mei Mosi ambapo kila mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani.

Alisema wafanyakazi wengi wamekuwa wakipata maslahi yao baada ya kustaafu kwa upendeleo kati ya mmoja na mwingine licha ya kuanza utendaji pamoja na kumaliza kwa mishahara inayolingana katika utumishi wa umma.

Mwenyekiti wa chama cha walimu mkoani Kagera CWT Costa Paul alisema  walimu 14 wa idara ya msingi na sekondari  kutoka halmashauri zote za mkoa huo watapatiwa vyeti na zawadi za wafanyakazi bora mwaka huu mkoani humo.

Alisema walimu hao waliteuliwa kwa kufanyiwa upembuzi wa vigezo vilivyotolewa na vyama vya wafanyakazi Tanzania TUCTA, baada ya kutimiza majukumu  kwa wakati, mahusiano mema  na watumishi wengine wakimwemo waajiri kuanzia ngazi ya kituo cha kazi.

Katika hatua nyingine Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUKTA )  mkoani Kagera Bw.Edward Mwisa ameiytaka serikali kuboresha maslahi ya wafanyakazi ikiwa ni pamoja na kuthamini mchango wa watumishi walioishia elimu ya darasa lasaba nchini.

Amesema watumishi hao ndio walioiweka madarakani serikali kuanzia awamu ya kwanza hadi awamu ya tano na wanaowaondoa kazini baadhi yao wamefundishwa na kuhudumiwa na waliohitimu darasa la saba katika sekta mbalimbali za kijamii.

Aidha ameitaka serikali kuhakikisha inaimarisha ulinzi na usalama wa wafanyakazi katika mkoa  wa Kagera, kanda ya ziwa na taifa kwa ujumla kutokana na vitendo vya mauaji ya watu wasiojulikana lakini pia unyanyasaji na utekaji unaoendelea dhidi ya watumishi.Hata hivyo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ambaye ni mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw.Deodatus Kinawilo kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa kagera Meja mstaafu Salum Kijuu amesema serikali itaendelea kuboresha maisha ya watumishi na kuongeza  ajira katika sekta ya elimu, afya na ngazi za halmashauri kote nchini.

Aidha amewataka watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia Maadili ya Utumishi wa umma,uwajibikaji na kuungana katika maboresho yanayofanywa na serikali ya kuingizwa kwenye mifuko ya pamopja na hifadhi ya jamii ili kukuza uchumi wa Viwanda.

Post a Comment