habari Mpya


Maafisa Idara ya Uhamiaji Mahakamani kwa Tuhuma ya kushambulia Wakazi wa Kabanga wilayani Ngara.

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini Tanzania Dr Anna Peter Makakala akiwa wilayani Ngara,mkoani Kagera –Picha na Maktaba yetu.

Maafisa Watano wa Idara ya Uhamiaji Wilayani Ngara Mkoani Kagera wamefikishwa Mahakama ya wilaya hiyo kwa tuhuma za kufanya shambulio kwa wakazi wa kata ya Kabanga wakitekeleza majukumu ya kuwasaka Wahamiaji haramu.

Mbele ya hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Ngara Andrew Kabuka mwendesha mashtaka wa Jeshi la Polisi Jumanne Maatu amesema Maafisa hao wametenda kosa hilo May 2,2018 katika mji wa Kabanga na kufanya vitendo vya udhalilishaji kisha kupora Mali za raia ambayo thamani yake haijajulikana.

Bw. Maatu amewataja watuhumiwa hao kuwa ni John Johannes  mwenye miaka 29, Joseph Richard  mwenye miaka 32, Hussein Mungunji   mwenye miaka 30, Johakimu Joseph  miaka 33 na Said Ally  mwenye umri wa miaka 38 na kwamba wote wanatuhumiwa kutenda kosa la jinai kwa kuvunja  kifungu cha sheria namba 241 sura ya 16 ya mwaka 2002.

Hata hivyo watuhumiwa wote kwa pamoja wamekana shtaka linalowakabili kwa kesi namba 115 na 116 ya mwaka 2018 na wako nje kwa dhamana ambapo hakimu wa mahakama ya wilaya Andrew Kabuka ameahirisha kesi yao hadi May 18,2018 itakaposikilizwa tena. 

Post a Comment

0 Comments