habari Mpya


Wakimbizi Sita Raia wa Burundi waliokufa Ajalini Ngara wazikwa Benaco.

Watu Sita ambao ni Wakimbizi kutoka Burundi waliofariki kwa ajali ya gari  Machi 29,2018 majira ya saa 10 jioni eneo la mteremko wa K9 kijiji cha Kasharazi wilayani Ngara mkoani Kagera iliyohusisha mabasi mawili kati ya msafara wa mabasi nane yaliyokuwa yamebeba Wakimbizi raia wa Burundi kutoka kambi ya Nduta wilayani Kibondo mkoani Kigoma kuelekea nchini mwao, wamezikwa leo April 2,2018  katika Makaburi ya Benaco, kijiji cha Rwakalemela Kata ya Kasulo wilayani Ngara.


Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia General Mstaafu Emmanuel Maganga wakati wa mazishi hayo,amewataka wakimbizi raia wa Burundi waishio kwenye makambi hapa nchini kutokatishwa tamaa na mtu yeyote katika kuhiyari kurejea nchini Burundi kwani kwa sasa kuna amani ya kutosha.

Brigedia General Mstaafu Maganga pia amewasihi wakimbizi kuchukulia ajali iliyotokea kama sehemu ya maisha huku akiyataka mashirika yanayowasafirisha wakimbizi hao kuchukua tahadhari na kuhakikisha vyombo vyao vinakuwa imara.

Wakimbizi hao waliofariki dunia na kuzikwa ni Tyisenge Minani, Nyabenda Leonia, Nyandwi Veronica, Miburo Gervas, Barutwanayo Salvatory na Buchumi Casmir na Shughuli hiyo ya mazishi imehudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali na Mashirika yanayohudumia Wakimbizi akiwemo Mwakilishi wa Shirika la UNHCR hapa nchini Tanzania, Bi. Chansa Kapaya.

Katika ajali hiyo Pia walifariki Watanzania wawili ambao ni Osilia Mabuye aliyekuwa Mfanyakazi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM na Mkazi wa Kijiji cha Kasharazi aliyepamiwa na basi lililopoteza mwelekeo baada ya kufeli mfumo wa breki na kusababisha ajali.
Aidha mpaka sasa Majeruhi waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Nyamiaga wote wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika na wamesafirishwa kurejea makwao nchini Burundi wakati katika Hospitali ya Murugwanza wakibaki majeruhi watatu (zote za wilayani Ngara mkoani Kagera ) huku waliopata rufaa kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando Jijini Mwanza wapo Wakimbizi Majeruhi 25.

Post a Comment

0 Comments