habari


UNHCR yawashukuru Wafanyakazi wa Hospitali za Nyamiaga na Murgwanza wilayani Ngara.

Mwakilishi wa Shirika la kuhudumia wakimbizi hapa nchini Bi. Chansa Kapaya, amewashukuru wafanayakazi wa hospitali za Nyamiaga na Murgwanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, kwa huduma na ushirikiano walioonesha kwa majeruhi wa ajali ya basi.

Bi. Kapaya ameyasema hayo Aprili 03, 2018, wakati wa mazishi ya wakimbizi sita walioaga dunia kwa ajali ya basi, iliyotokea Machi 29, 2018 katika kijiji cha Kasharazi, wakitokea katika kambi ya wakimbizi ya Nduta wilayani Kibondo mkoani Kigoma na kuzikwa Benaco Ngara.

Alisema shirika la kuhudumia wakimbizi, kwa kushirikiana na mashirika mengine, wamejitahidi kuokoa maisha ya majeruhi, ikiwa ni pamoja na kukodi ndege ya kuwasafirisha waliopewa rufaa kwenda hospitali ya Bugando.

Tunawashukuru wahudumu wa hospitali za Nyamiaga na Murgwanza, pamoja na serikali ya wilaya, na kwa namna ya pekee wanakijiji cha Rwakalemela, waliotoa eneo la kuwahifadhi wenzetu; Mwenyezi Mungu awabariki.” Alisema Bi. Kapaya.

Aidha, Mkurugenzi wa Idara ya Kuwahudumia Wakimbizi Wizara ya Mambo ya Ndani hapa Nchini Bw. Harison Mseka, alisema kwamba jumla ya wakimbizi 21,000, wamerejea nchini Burundi kutoka kwenye kambi za wakimbizi mkoani Kigoma tangu Septemba 2017.

Alisema kila wiki wakimbizi 2,000 wanatakiwa kurejea nchini Burundi, sawa na 8,000 kwa mwezi, na kuongeza kwamba mwaka jana walilenga kurejesha wakimbizi 12,000, lakini walifanikiwa kuwarejesha wakimbizi 13,300.

Bw. Mseka alisema mwaka huu wanalenga kuwarejesha wakimbizi wapatao 80,000, ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano waliojiwekea kwa mwaka huu.
Amefafanua kwamba majeruhi 26 wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Murugwanza, na Hospitali ya rufaa ya Bugando Mwanza, ambapo wengine wako katika kambi ya Lumasi.

Post a Comment