habari


Mvua yasababisha Shule Tatu za Msingi Kahama Kufungwa .

Mvua ya April 18,2018 mjini Kahama,mkoani Shinyang'a ilinyesha  na kusababisha baadhi ya maeneo kukumbwa na mafuriko , kusababisha barabara na nyumba nyingi kujaa maji.

Mvua hiyo pia imesababisha hasara kubwa ya uharibifu wa mali.  

Picha/Habari na  Simon Dioniz-Radio Kwizera Kahama 97.7 Fm.

Baadhi ya wakazi wa kata za Mungula, Nyahanga, Majengo, Nyasubi Malunga na Muhongolo katika halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani Shinyanga wamekosa mahali pa kuishi kufuatia nyumba zao kujaa maji kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia jana.


Wakiongea na Radio Kwizera baadhi ya wakazi wa kata ya Muhungula na kata ya Majengo wamesema kuwa Mvua hiyo imesababisha nyumba zao kuanguka na mpaka sasa wamelazimika kuhamisha watoto na familia kwa majirani.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya mji wa Kahama Bw. Andarson Msumba amekiri kupokea taarifa za maeneo hayo na kwamba wanachokifanya ni kuangalia namna ya kufumua maeneo yaliyoziba ili maji yaweze kupita.

Hata hivyo kutokana na mvua hizo, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama imezifunga shule 3 za msingi kutokana na shule hizo kukumbwa na mafuliko na madarasa kujaa maji na hivyo kusababisha wanafunzi kushindwa kwenda shule.

Afisa Elimu katika halmashauri ya Msalala wilayani Kahama Bw. Julias Bubelwa amesema shule zilizofungwa ni pamoja na shule ya Msingi Matinje, Kadati na Izuga ambazo zimefungwa hadi Apri 29 mwaka huu.

Post a Comment