habari


Madaktari Bingwa waendesha Zoezi la Upasuaji Mdomo Sungura Hospitali ya Misheni Rulenge,Ngara.

Madaktari Bingwa wakifanya upasuaji wa Mdomo wazi wakati wa zoezi hilo katika Hospitali ya Misheni Rulenge wilayani Ngara mkoani Kagera Leo April 18,2018.

Ngara. Na Shaaban Ndyamukama Radio Kwizera Ngara.

 Uongozi wa Jimbo katoliki la Rulenge Ngara mkoani Kagera umeendelea kutoa huduma ya upasuaji watoto wenye midomo Wazi ama midomo sungura katika Hospitali ya misheni Rulenge, baada ya kukamilisha zoezi hilo Hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo mkoani humo.

Askofu wa jimbo hilo Mhashamu Severine Niwemugizi alisema huduma hiyo inatolewa na madaktari bingwa kutoka nchi za Uganda na Rwanda wakisaidiana na madaktari wa hospitali zinazomilikiwa na jimbo hilo.

Askofu Niwemugizi alisema huduma hiyo inatolewa bure na wazazi wanaoleta watoto wao wanapatiwa gharama za usafiri na huduma ya chakula na kwamba zoezi hilo linatarajia kukamilika ifikapo Jumapili ya April 22, mwaka huu.


Alisema huduma hiyo inafadhiliwa na shirika la kuhudumia watoto wenye midomo Sungura kwa majimbo ya kanisa katoliki katika nchi mbalimbali likiwemo jimbo la Rulenge Ngara na hiyo ni awamu ya nne tangu kuanza jimboni humo.

Tunachohimiza wazazi na walezi wasione kuzaliwa watoto hao kuwa wamelogwa wakajiingiza kwenye imani za kishirikina wakiwahi kuwaona mtaalamu wa afya watawaelekeza na kuwahudumia na kuwa hali ya kawaida”Alisema Niwemugizi.

Pia alitoa hamasa kwa serikali kutoa huduma hiyo kwa watoto hao kama makundi mengine ya walemavu kwani wazazi wenye watoto wa midomo sungura hawana gharama za kuwapeleka hospitali kufanyiwa upasuaji.

Aidha mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Rulenge Dkt Prosper Malya alisema kfikia jana walisajili watoto 17 kutoka ndani na nje ya jimbo hilo na kufikia jana April 17, 2018 jioni watoto 11 wenye midomo sungura walifanyiwa upasuaji.

Dkt Malya alisema sababu za kuzaliwa watoto wenye midomo sungura inasababishwa na vinasaba kiukoo, mama kubeba ujauzito katika umri mkubwa, magonjwa ya pumu na ukosefu wa lishe wakati mama akiwa mjamzito.

Alisema malengo ni kuhudumia watoto 30 kwa wiki ambapo katika awamu tatu ziizopita katika Hospitali  teule ya wilaya ya Biharamulo walipatikana watoto 40 na wote hakuna hata mmoja aliyepoteza maisha wala kuwa na afya dhaifu.

 “Utumiaji wa pombe kupita kiasi, uvutaji wa tumbaku na matumizi ya ugoro huweza pia kuchangia kuzaliwa watoto wenye midomo sungura lakini wakifanyiwa upasuaji wanakuwa hali ya kawaida”. Alisema Dkt Malya.

 Pia alitoa wito kwa wananchi wenye watoto wa namna hiyo kujitokeza kupata huduma ambayo haina gharama katika zoezi hilo ingawa katika hospitali nyingine huweza kugharimu Sh1.2 milioni kwa upasuaji wa mtoto mmoja.

 Alisema waliojitokeza kuhudumiwa wametokea Chato, Geita, Burundi Biharamulo na maeneo jirani ya Rulenge na kwamba wanahamasishwa wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma bila kutumia gharama zao.

Post a Comment