habari Mpya


Kakonko Wahitaji Wataalam wa Miamba.

.com/proxy/
Wananchi wa Wilaya ya Kakonko, Mkoani Kigoma, wameiomba Serikali isaidie kuwapatia wataalam wa miamba, ili wafanye utafiti utakaobainisha kiasi cha madini yaliyogundulika kuwepo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
 
Akiwasilisha Taarifa ya Wilaya hiyo kwa Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo, aliyefika ofisini kwake na kuzungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama, akiwa katika ziara ya kazi jana Machi Mosi, Mkuu wa Wilaya Kanali Hosea Ndagala alisema kuwa Madini ya Dhahabu yamegundulika katika maeneo mbalimbali, hususan Nyamtukuza, Kasuga na Muhange lakini haijaweza kufahamika ni kiasi gani kilichopo.
 

“Tunakuomba utusaidie upatikanaji wa wataalam ili kujua takwimu sahihi za kiasi cha Madini hayo kilichopo kwenye maeneo yaliyogundulika.” alisema Ndagala.
 
Aidha, Kanali Ndagala alitaja changamoto nyingine katika Wilaya hiyo kuwa ni uwepo wa hazina kubwa ya Madini ya Chokaa katika Hifadhi ya Pori la Akiba la Moyowosi, lakini imekuwa vigumu kufanya shughuli za uchimbaji kutokana na Sheria za Hifadhi.
 
“Kwa namna ya pekee tunakuomba utusaidie eneo hilo litolewe ridhaa ya kufanyika shughuli za uwekezaji na uchimbaji ili kuharakisha maendeleo ya uchumi wa viwanda, kutoa nafasi za ajira na kuinua vipato vya wananchi katika wilaya yetu,” alisema.
 
Akijibu maombi husika, Naibu Waziri Nyongo alisema kuwa Serikali kupitia Wizara yake, hivi sasa imejipanga kufanya tafiti mbalimbali za Madini nchini kote kwa kuwatumia wataalam wa jiolojia kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST).
 
Akifafanua zaidi, alisema kuwa lengo la Serikali ni kuweza kuainisha maeneo yote yenye madini, kutoa ushauri na hata kukaribisha wawekezaji kuwekeza katika maeneo husika kwa maana ya kuwapa taarifa sahihi za kijiolojia.
 
“Hivyo basi, tutawaelekeza wataalam wetu wafike hapa Kakonko pia na kufanya utafiti,” alisema Nyongo.
 
Kuhusu upatikanaji wa Madini ya Chokaa katika eneo la Hifadhi, Naibu Waziri aliahidi kulifanyia kazi suala hilo ili kuona kama kuna uwezekano wa kutolewa ridhaa ya kuchimbwa Madini hayo kwani alisema yanahitajika sana kwa sasa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.
 
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri alieleza kuwa, kutokana na Mheshimiwa Rais John Magufuli kuifanya Wizara ya Madini kujitegemea na kusimama peke yake, kutoka iliyokuwa Wizara ya Nishati na Madini; jukumu la Wizara hiyo mpya sasa ni kuhakikisha Madini yanalinufaisha Taifa ipasavyo.
 
“Macho yetu sasa ni kwenye Madini tu. Tunataka kuhakikisha kwamba kila Mkoa hapa nchini unachangia katika Pato la Taifa kupitia shughuli za Madini kwani nchi yetu imejaaliwa kuwa na Madini mbalimbali katika Mikoa karibu yote.” alisema Nyongo.
 
Akielezea ziara yake katika Mkoa huo wa Kigoma, Nyongo alisema itahusisha pia kutembelea na kujionea shughuli za uchimbaji wa Madini Chumvi zinazofanyika Uvinza.
 
Akifafanua, alisema kuwa nchi imekuwa ikiagiza kiasi kikubwa cha Chumvi kutoka nje wakati Madini hayo yanapatikana hapa nchini, hivyo Serikali imedhamiria kuhakikisha inawezesha uzalishaji wa kutosha wa Chumvi bora hapa nchini itakayotosheleza mahitaji ya Soko la ndani.
 
Naibu Waziri Nyongo anaendelea na ziara yake ambayo itahitimishwa mkoani Kigoma. Mikoa mingine aliyotembelea katika ziara hiyo ni Mwanza, Geita na Kagera.
 
Na Veronica Simba, Kakonko

Post a Comment

0 Comments