habari Mpya


DC Ngara achangia Ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi Mukalinzi.

28876732_1783969984976237_1032833455_o
Mkuu wa wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mntenjele amekabidhi mabati 100 na misumari vyote vikiwa na thamani ya Sh 2.83 milioni kwa ajili ya  kuezeka kituo kidogo cha Polisi katika kijiji cha Mukalinzi , Kata ya Muganza wilayani humo ikiwa ni kutimiza ahadi yake ya kuunga mkono nguvu za wananchi wanaojitolea.
Kanali Mntenjele ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ngara amekabidhi mabati hayo  leo Machi 6 akitekeleza ahadi yake baada ya kutembelea kijiji  hicho mwezi Jana  akiwa katika ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.
 
Amesema wananchi wamehamasika kwa kuchangia nguvu zao na rasilimali zinazowazunguka na kujenga kituo cha polisi ambacho jengo lake limefikia hatua ya renta likihitaji vifaa vya viwandani kukamilika  na kuanza kutumika.

28822865_1783969974976238_1160364266_o
Mwenyekiti wa kijiji cha Mukalinzi Richard Magogoro alisema hali ya ulinzi na usalama inaridhisha baada ya kuletwa askari polisi kufanya kazi ya kutokomeza uhalifu kwa kushirikiana na wananchi kuimarisha amani na  utulivu.
 
Amesema ujenzi wa kituo cha polisi  unategemea kugharimu Sh15 milioni  pia  kila mwananchi anachangia Sh10 000 baada ya watu wengi  kuathiriwa na matukio ya ujambazi uliosababisha watu 17  kupoteza maisha  kati ya mwaka 2009 hadi 2016.
 
Matukio ya uhalifu yamesababisha  watu kupoteza maisha na wengine kuhama maeneo haya na baadhi walijeruhiwa na majambazi lakini tuliopo tumechangia Sh6 milioni na kituo hadi sasa kimegharimu Sh 9 Milioni” Amesema Magogoro.
 
Aidha  amesema  wananchi  wanaiomba serikali kuwajengea mnara wa mawasiliano kwani majambazi hutumia changamoto hiyo kuvamia kijiji kisha kuhatarisha  usalama wakijua hakuna taarifa  zinazoweza kupelekwa jeshi la polisi kwa haraka kupitia njia ya simu za mkononi.
 
Naye Mkuu wa polisi wa wilaya ya Ngara, Abeid Maige aliwahimiza wananchi kushirikiana na jeshi la polisi kwa kufanya doria za mara kwa mara na kutii sheria bila shuruti huku wakitoa taarifa dhidi ya watu wanaohofia kuhatarisha usalama.
 
Amesema kituo hicho kitahudumia vijiji vitatu vya kata ya Muganza lakini pia vijiji jirani vya Murubanga, Nyamagoma na Magamba vilivyopo kata ya Murusagamba na kwamba wajihadhari na kukaa na raia wa kigeni kutoka nchi jirani ya Burundi.
 
Kijiji cha Mukalinzi kata ya Muganza wilayani Ngara chenye wakazi 10,228 waishio katika kaya 1060 kinapakana na nchi jirani ya Burundi ambapo kimekuwa kikabiliwa na matukio ya ujambazi kwa baadhi ya watu kuuawa kwa risasi na wengine kujeruhiwa au kuhama makazi yao.

Post a Comment

0 Comments