habari Mpya


CCM Ngara yaitaka Serikali Kutumia Fedha za Ruzuku kwa Miradi ya Maendeleo.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ngara mkoani kagera kimeitaka Serikali kutuma fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo kwa wakati kuunga mkono nguvu za wananchi baada ya kuibuliwa ikiwa ndiyo vipaumbele katika utekelezaji wa ilani ya chama hicho.

Wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM wilayani Ngara wametoa wito huo March 2,2018  wakati wa mkutano mkuu wa kujadili utekelezaji wa ilani ya chama  hicho kwa mwaka 2017 katika miradi mbalimbali ya maendeleo   katika sekta ya kilimo, Mifugo ,afya, maji, barabara, elimu mazingira pia ulinzi na usalama hasa ukamilishaji wa vituo vya polisi vilivyotelekezwa.
Kutoka kushoto ni Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani Ngara mkoani Kagera Bw. Herman Hume aliye muwakilisha Mkurugenzi Mtendaji katika mkutano huo, wapili ni Katibu tawala wa wilaya ya Ngara,Bw.Vedastus Tibaijuka ,watatu ni Mwenyekiti CCM (W) Bw. George Rubagora na wa nne ni Katibu CCM (W) Bi. Mwajemi Baragama.

Wajumbe hao walisema kero kubwa ya wananchi ni kutokamilika miundombinu katika sekta hizo kwa kujenga vyumba vya madarasa, nyumba za watumishi, zahanati na vituo vya afya na kutatua  migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji au wenye uwezo kifedha na maskini.

Mwenyekiti wa CCM wilayani Ngara George Rubagola alisema miradi ya maji ya benki ya dunia imekwama katika vijiji ilikoelekezwa na wanaoteseka ni wanafunzi, wazee, watoto wadogo katika familia na wanawake kwa kutumia maji yasiyosafi na salama kisha kuhatarisha afya zao.

Rubagola alisema halmshauri haina budi kuongeza juhudi za kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuepuka kusubiria utozaji wa ushuru wa mazao kwa wafanyabiashara au  walanguzi kwenye magulio na vibanda vya ujasiriamali wanaotegemea mapato yao madogo kujikwamua kiuchumi.

"Ujenzi wa miundombinu katika huduma za kijamii imefikia asilimia 34 kufikia Desemba 2017 na imekwama baada ya serikali kushindwa kutekeleza ilani ya chama tawala na falsafa ya Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa CCM taifa ya hapa kazi tu" Alisema Rubagora.
Mjumbe akichangia moja ya Hoja katika Kikao hicho.

Alisema Halmashauri iliidhinishiwa na serikali kupata Sh 45.88 bilioni kwa mwaka 2017/2018 lakini fedha ambayo ilishapokelewa hadi Desemba 2017 ni Sh13 bilioni  ambapo utekelezaji wa miradi iliyoibuliwa  kiuhalisia iko chini ya malengo licha ya uchangiaji wa vifaa kwenye maeneo yao

Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya wilaya ya Ngara, Bw. Ghalibu Mkumbo alisema katika bajeti ya mwaka 2017/ 2018 katika robo ya pili kufikia Desemba 31,2017 Halmashauri hiyo ilikusanya Sh 520 milioni  kati ya Sh 2.03 bilioni kutoka vyanzo vya ndani na utekelezaji wa miradi mbalimbali imefikia asilimia 34 kiuhalisia kisha kuwepo miradi mingi kubaki viporo

Hata hivyo Mkumbo alisema  halmashauri kwa fedha zinazopatikana kutoka serikalini imeboresha miundombinu katika sekta ya Afya kwa kukarabati zahanati na vituo vya afya vyumba vya madarasa   pamoja na barabara lakini  changamoto ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maji ambayo imetelekezwa tangu kuanzishwa mwaka 2012.

 Katika mafanikio yaliyopo sekta ya kilimo  imejikita katika zao la biashara la kahawa kwa kusambaza miche kwa wakulima huku idara ya mifugo iijihusisha na upigaji chapa ng'ombe na kuchanja mifugo mingineyo kupunguza magonjwa mbalimbali” Alisema Mkumbo.

Afisa  Kilimo Costantine Mudende  alisema   wilaya ya Ngara inayo mibuni ya kahawa 2,671,805  kati yake ni 1,113,960, ni aina ya  arabika na 1557, 845 ni aina ya robusta,  kwa wakulima wa kahawa 8,756 na kwamba idara imesambaza miche 72,065  yenye thamani ya Sh80 milioni katika kata 20 kutoka  chuo cha utafiti wa mazao cha Maruku mkoani Kagera

Kwa upande wa Afisa mifugo Richard Ngowi alisema  jumla ya ng’ombe 68,713 katika vijiji 75 wamepigwa chapa kati ya ng'ombe 78,000 waliosajiliwa kwa wafugaji 5,197 ambapo idara ilikuwa imelenga kupiga chapa ng'ombe 75,000

Pia alidai kwamba kati ya January hadi December 2017 jumla ya Ng'ombe 886 walichanjwa dhidi ya ugongwa wa ndigana kali katika kijiji cha Rwakalemela  pia ng'ombe 12,239, walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa  miguu na midomo, (FMD) katika kijiji cha Kasulo.
Vile vile alisema ng'ombe 2452 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa chambavu (BQ) na ng'ombe 4,167 walichanjwa dhidi ya homa ya mapafu (CBPP) Katika vijiji vya Rwakalemela na Nyakariba kata ya Kasulo ambapo  kuku 56, 058 walichanjwa dhidi ya ndondo na kuku 4532 walichanjwa dhidi ya ugonjwa wa ndui katika mitaa ya Ngara mjini na kijiji cha Nyamiaga.

Hata hivyo katibu tawala wa wilaya ya Ngara Vedastus Tibaijuka   aliwataka wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM kila kata kuhamasisha wananchi kuchangia miradi ya maendeleo wakati halmashauri ya wilaya na serikali kwa ujumla ikitafuta vyanzo vya mapato kuboresha  miundombinu ya kutoa huduma bora za kijamii.

Post a Comment

0 Comments