habari Mpya


NEC yasema Uchaguzi Mdogo, kufanyika Februari 17,2018.

NEC_1514998781-1600x705
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmod Hamid.
 
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imesema kuwa uchaguzi mdogo katika majimbo ya Siha mkoani Kilimanjaro na Kinondoni mkoani Dar es Salaam pamoja na Kata nne za Tanzania Bara utafanyika Februari 17, 2018 kufutia waliokuwa Wabunge katika majimbo hayo kujivua uanachama na kukosa sifa za kuendelea kuwa  Wabunge.

Kwa mujibu wa taarifa ya Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mkuu mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmod Hamid imeeleza kuwa pamoja na majimbo  hayo, pia kata nne za Isamilo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Manzase,  Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Madanga Halmashauri ya Wilaya ya Pangani mkoani Tanga na Kimagai Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma zitafanya uchaguzi mdogo .
 
Jaji mkuu huyo mstaafu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid amesema kuwa, tume hiyo itaendesha uchaguzi huo baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Job Ndugai kuhusu  Jimbo la Kinondoni jijini Dar es Salaam na Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro kuwa wazi.
 
Jaji Mahmoud amesema kuwa, barua hiyo ilieleza kuwa majimbo hayo yapo wazi baada Maulid Mtulia aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kinondoni kujivua uanachama wa CUF na Dkt. Godwin Mollel wa Jimbo la Siha kujiuzulu uanachama wa CHADEMA na hivyo wote kukosa sifa za kuwa wabunge.
 
Pia, ameeleza kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa ikiitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika kata nne za Tanzania Bara.

Post a Comment

0 Comments