habari Mpya


Picha za Ujenzi mradi wa Umeme Rusumo,Ngara/Kagera.

Ujenzi huo wa mradi wa kuzalisha na kusambaza umeme wa maji wa megawati 80 katika maporomoko ya maji ya Rusumo katika Mto Kagera unafanyika katika eneo la Rusumo wilayani Ngara,mkoani Kagera na  utanufaisha nchi tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.


Ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme unagharimiwa na Benki ya Dunia ilhali ujenzi wa njia ya umeme kuunganisha katika Gridi za Taifa za nchi hizo tatu unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari .


Kupitia kwa mpango huo kabambe, kila nchi itapata nyongeza ya megawati 26.6 katika gridi zao za taifa na hili linatarajiwa pia kuimarisha uunganishwaji umeme wa kikanda baina ya nchi hizo tatu ambazo pia ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Kukamilika kwa mradi huu kutanufaisha kaya elfu saba (7,000) kupitia mpango wa maendeleo katika serikali za mitaa na kaya nyingine 188 zinazozunguka mradi huu,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza kuwa inategemewa pia wakati wa utekelezaji wa mradi huu kabambe wa kikanda katika eneo la Afrika Mashariki, kutakuwa na ajira kwa zaidi ya wafanyakazi 500 wenye weledi, weledi wa kati na vibarua kutoka nchi tatu zitakazonufaika na mradi huu.
Ujenzi wa mradi unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka mitatu na utakamilika mwaka 2020. 
Makandarasi wawili kutoka China, CGCOC Group Ltd na Jiangxi Water & Hydropower Construction Company Ltd (CGCOC - JWHC JV) watajenga bwawa la maji pamoja na miundombinu mingine.
Kwa upande mwingine, muunganiko wa makandarasi wawili Rusumo Falls Andritz Hydro GmbH ya Ujerumani na Andritz Hydro PVT Ltd ya India watahusika na ufungaji wa mitambo ya kuzalisha na kusambaza umeme.
Mradi wa kuzalisha umeme wa maji wa Rusumo unasimamiwa na taasisi ya Nile Equatorial Lakes Subsidiary Action Program Co-ordination Unit (NELSAP-CU) iliyopewa jukumu hilo na nchi tatu wanufaika kupitia Kampuni ya Rusumo Power Ltd (RPCL), inayomilikiwa kwa pamoja na mashirika ya umeme katika nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

Post a Comment

0 Comments