habari Mpya


Msaada Wahitajika baada ya Maafa ya Mvua Kagera.

Mvua iliyoambatana na upepo mkali, kwa mara nyingine imeleta janga lingine mkoani Kagera na kuacha wasiwasi kwenye maeneo kadhaa ya mkoa huo ambao hali ya hewa kwasasa inaonesha mawingu mazito yanayoashiria kuendelea kwa mvua hizo.

Wilaya ya Muleba iliyopo mkoani Kagera Siku ya Jumanne imekumbwa na mvua iliyoambatana na na upepo mkali huku wenyeji wakiita kuwa ni kimbunga, kitendo kilichosababisha nyumba zaidi ya 30 kuanguka na nyingine kadhaa kuezuka paa, mashamba ya migomba kwenye zaidi ya hekari 35 kuanguka na kuacha hofu kubwa kwa wananchi.

Mwandishi wa mtandao huu ametembelea maeneo yaliyoathirika na kuzungumza na wananchi walioguswa na hali hiyo katika kata za Mubunda, Buganguzi na Ibuga, ambapo wameeleza kuwa mvua hiyo ilinyesha ghafla muda wa mchana na kusababisha athari hizo, huku watoto wakiogopa na kukimbia hovyo kutokana na hofu ya kuona migomba ikianguka na nyumba zao.

Miongoni mwa miundombinu iliyoharibika ni pamoja na shule ya Mkembe Sekondari ambayo darasa zima zimeezuliwa na upepo.

Aidha wamesema kuwa wameweza kushirikiana na majirani zao ambao hawajaguswa na dhahama hiyo kwa kuwapatia hifadhi ya muda, wakati wakisubiri kuangalia jinsi ya kurudishia hali zao.

Wametumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuwasaidia kwa muda walau chakula la malazi, katika kipindi ambacho wanaendelea na mchakato wa kurudishi mazingira yao.

Itakumbukwa kuwa mwezi mmoja uliopita, mtu mmoja alifariki dunia kwa kula chakula kilichosadikiwa kuwa na sumu katika kata hizo, na kusababisha watu wengine zaidi ya 80 kulazwa kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati wilayani humo.

Post a Comment

0 Comments