habari Mpya


Ufaransa yatoa msaada wa Mil 636 kusaidia mradi wa utoaji fedha taslimu kwa Wakimbizi Tanzania.

Serikali ya Ufaransa imetoa mchango wa EUR 250,000 (Tsh. 636 milioni) kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ili wakimbizi wanaoishi nchini Tanzania wapate msaada zaidi wa fedha taslimu. 

Mchango huu unafuatia ule wa EUR 750,000 za mwaka jana, huu ukiwa uthibitisho wa utayari wa Serikali ya Ufaransa katika kuimarisha njia za kuleta usalama wa chakula na ujumuishi.

Mwezi Desemba 2016, WFP ilianza kutoa TSh 20,000 (Dola za Marekani 9.00) kila mwezi kwa wakimbizi 10,000 kama sehemu ya programu ya majaribio inayotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi  (UNHCR). 

Mchango wa Ufaransa unaiwezesha WFP kuendeleza programu ya fedha taslimu kwa wakimbizi 10,000 kwa miezi miwili ya nyongeza.

Kupitia programu hii, wakimbizi wanapata mgao wa mafuta ya mbogamboga yaliyoongezewa virutubisho na mchanganyiko maalumu wa uji, wakati ambapo badala ya mgao wa mahindi, kunde na chumvi wakimbizi wanapewa fedha taslimu. 

Kabla ya kuzinduliwa kwa programu ya fedha taslimu, wakimbizi walikuwa wakipewa tu msaada wa chakula kutoka WFP.

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni, asilimia 98 ya kaya zinazoshiriki katika mpango huu zinapendelea fedha taslimu badala ya migao ya chakula, wakati ambapo asilimia 83 walisema utaratibu huu umeongeza ubora wa milo yao na uchaguzi mpana wa aina ya vyakula.

“Msaada wa Ufaransa kwa mradi huu ni muhimu,” alisema Bi. Malika Berak, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania. “Mfumo huu utawezesha kuwa na utoaji msaada wa chakula wenye ufanisi, unaoheshimu soko la bidhaa la mahalia na litakaloacha alama nzuri kwa mazingira.”

Msaada wa fedha taslimu una manufaa ya nyongeza katika kuunda soko imara kwa wakulima na wafanya biashara wa mahalia, na wakati huo huo ukiwapatia wakimbizi na wanufaikaji wengine uhuru wa kuchagua nini wanunue, wapike na kuzilisha familia zao.

“Kufuatia ubunifu katika njia za utumaji fedha taslimu, msaada wa fedha taslimu umeonekana siyo tu kuwa ndio unaopendelewa zaidi kwa wakimbizi kupokelea msaada wa chakula, bali pia kama njia yenye ufanisi inayokuza uchumi wa mahalia,” alisema Michael Dunford, Mwakilishi Mkazi wa WFP Tanzania na kuongeza.

“Utumaji wa fedha taslimu na ongezeko la shughuli za kiuchumi kunaweza kusaidia kuimarisha miundombinu ya mahalia, kama vile huduma za fedha, huduma za masoko, na pia upatikanaji wa mitandao ya intaneti na simu.”

Katika miaka ya karibuni, WFP imekuwa ikiongeza kiasi cha msaada inaotoa kwa njia ya fedha taslimu na vocha. Kote ulimwenguni, asilimia 29 ya wanufaikaji wa WFP wanapokea msaada wa chakula kwa njia ya utumaji wa fedha taslimu.

Tangu kutokea kwa machafuko nchini Burundi mwaka 2015, karibu Warundi 250,000 wametafuta hifadhi nchini Tanzania, ambayo hivi sasa imewapa hifadhi wakimbizi 315,000, wengi wao wakiwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Hadi mwisho wa mwaka, WFP inalenga kupanua programu yake ya utoaji fedha taslimu ili kuwafikia wakimbizi 80,000. WFP inahitaji jumla ya Dola za Marekani milioni 6.8 kwa mwezi ili kuendelea kutoa msaada wa fedha taslimu na chakula kwa wakimbizi nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments