habari Mpya


Rais Magufuli Amtaka Muhongo Ajitathimini , ikiwezekana aachie ngazi haraka.

Waziri Prof. Muhongo –Picha na Maktaba yetu.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo Jumatano, Mei 24, 2017 wakati wa kupokea Ripoti ya Kamati Maalum ya Utafiti wa Mchanga (Makanika) uliomo kwenye makontena yaliyozuiliwa kwenye bandari tofauti hapa nchini, pamoja na hatua nyingine, amemtaka Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ajitathmini kwa kina na kuchukua hatua na ikibidi ajiuzulu mara moja kufuatia kushindwa kusimamia suala la mchanga wa madini unaosafirishwa kwenye makontena.

 Akipokea ripoti hiyo, Rais Magufuli pia amemfuta kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), na kuivunja bodi hiyo kwa upotevu wa madini huku akiitaka TAKUKURU na vyombo vya dola kuwachunguza na kuwachukulia hatua wafanyakazi wa bodi hiyo.

Aidha Rais Magufuli ameonesha kusikitishwa mno na ripoti hiyo ambayo imebainika kwamba kiwango kikubwa cha madini kinachotoroshwa nje ya nchi.

Ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinalinda madini yasitoroshwe na amepiga marufuku usafirishwaji wa mchanga huo nje ya nchi.

Rais Magufuli amesema hayo baada ya kupokea ripoti ya kamati iliyokuwa ikichunguza suala la mchanga kwenye makontena .

Kamati hiyo ya wataalamu wa jiolojia na uchambuzi wa kisayansi iliyoundwa Machi 29 mwaka huu,2017 ilichunguza aina ya madini yaliyopo, kiasi na viwango vya ubora.
Rais Dkt. John Magufuli.

Akikabidhi ripoti hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Mruma amemueleza Rais Magufuli kuwa makontena yaliyofanyiwa utafiti ni 277 ambapo Kamati yake imebaini kuwepo na ufisadi mkubwa kwenye suala la usafirishaji wa mchanga huo, ambapo kiwango kikubwa cha dhahabu kimekuwa kikitoroshwa kwenye mchanga huo.

“Kamati imebaini kuwapo kwa kiwango kikubwa cha dhahabu kwenye makontena ambapo kontena moja lina wastani wa kilogramu 28 za dhahabu ambapo thamani yake kwenye makontena zaidi ya 277 yaliyozuiwa bandarini ni kati ya Tsh bilioni 676 hadi trilioni 1.14.”

“Makinikia hayo yalikutwa pia na madini ya shaba, silva, chuma na shaba. Kiwango cha Silva kilikuwa 6kg-7kg kwa kontena moja hivyo kufanya jumla ya 1689kg kwa makontena 277 yaliyozuiwa bandarini.”

“Licha ya madini mkakati (strategic metals) kuwapo katika makinikia, hazikuwa zikifahamika na kusababishia serikali hasara.”

“Kamati imesema mashine ya ukaguzi wa makontena ina matatizo kwani walificha chuma ndani ya makontena na mashine haikuona. Sababu mashine za ukaguzi bandarini hazifanyi kazi vizuri, huenda njia hiyo ilitumika pia kutorosha meno ya tembo.”

“Kamati imependekeza makontena yapimwe vizuri ili kuweza kubaini aina na thamani za madini yote yaliyomo kwenye mchanga.

Kamati imependekeza watumishi wa TMAA na Wizara husika wanaohusika na upotevu wachukuliwe hatua.” alisema Mwenyekiti huyo.

Aidha  Mwenyekiti wa Kamati alimkabidhi Rais Magufuli nakala 5 za ripoti hiyo ambapo amemwambia baadhi ya mambo akiyasoma yatamkera.

Post a Comment

0 Comments